Exodus 1:8-22

8 aKisha mfalme mpya ambaye hakufahamu habari za Yosefu akatawala Misri. 9 bAkawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kutuliko sisi. 10 cNjooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana dhidi yetu na kuondoka katika nchi hii.”

11 dBasi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. 12Lakini walivyozidi kuteswa ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi; Wamisri wakawaogopa Waisraeli, 13 ekwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. 14 fWakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.

15 gMfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Kimisri waliowazalisha wanawake wa Kiebrania, ambao majina yao ni Shifra na Pua, 16“Mtakapowazalisha wanawake wa Kiebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni, lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.” 17 hLakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi. 18Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?”

19 iWakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania ni tofauti na wanawake wa Kimisri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.”

20 jKwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi. 21 kKwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.

22 lKisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”

Copyright information for SwhNEN